Burundi : Je, Waziri Ndirakobuca anajaribu kuteka nyumba ya aliyekuwa Msuluhishi wa taifa ?

Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca ameripotiwa kuongeza vitisho kwa familia ya aliyekuwa Msuluhishi wa taifa marehemu Mohammed Rukara kwa zaidi ya miezi miwili. Alipokufa zaidi ya miaka mitatu iliyopita, Mohammed Rukara aliacha, pamoja na vitu vingine, nyumba iliyoko mbele ya ile ya Waziri Mkuu kwenye kitongoji cha Mutanga Sud, sekta ya Rohero, wilayani Mukaza, jijini Bujumbura. Tangu kutawazwa kua Waziri Mkuu, Gervais Ndirakobuca ameendelea kupanua eneo aliloliteka ndani ya makazi ya majirani zake. (Le Mandat)

Kontena ambamo polisi wanaomulinda wanalala, Waziri Mkuu Gervais Ndirakobuca aliliweka katika nafasi iliyopo kati ya barabara ya lami na nyumba ya familia ya marehemu Mohammed Rukara Khalfan. Ukuta ulibomolewa kwa sehemu ili kuruhusu kusimika kontena hilo kubwa linaloweza kusogezwa. Karibu na kontena, jiko la polisi hawo limejengwa. Huko pia, ilihitajika kuharibu sehemu ya ukuta wa makazi ya familia ya marehemu Mohammed Rukara, ambayo yanalindwa na walinzi, bila kuuliza yeyote. Kama sehemu ya uimarishaji wa usalama wake tangu kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu, kijijumba cha chuma cha mbwa watatu kiliwekwa pia kwenye hayo makazi ya majirani zake. Kutokana na uvamizi na uharibifu wa makazi hayo, familia ya marehemu Mohammed Rukara ililazimika kuanza kutafuta wateja ili kuuza nyumba ile. Kulingana na vyanzo vya habari vya kwa shirika la habari Le Mandat, bei ya nyumba ilikuwa faranga za Burundi bilioni nne .

Wateja waliogopa

Nyumba ya familia ya Rukara iliyoko kwenye barabara iitwayo Avenue de la dynastie na ile ya waziri mkuu zimetenganishwa na barabara ya lami ambayo kwa sasa inafanyiwa ukarabati.

Kufika huko, waliokuja kutizama biashara walitishwa na wingi wa askari polisi, kizuizi upande wa pili wa lami, mbwa na uharibifu wa makusudi wa “majirani hao wa ajabu”. Kuna wengine ambao wametoa chini ya bei iliyowekwa na familia ya Rukara. Mmoja wa wale waliojaribu kununua nyumba ile alituambia : “Jumla ya pesa nilizopendekeza zilikua zinatosha kwa maoni yangu kwa sababu ni, kwa vyovyote vile, misheni ya kujitoa muhanga.” Vyanzo vyetu vya habari vinaeleza kuwa, baada ya hapo, Waziri Mkuu alipata taarifa kwamba nyumba ile inauzwa na akamtuma mjumbe kupendekeza kwenye familia ya Rukara faranga bilioni mbili. Familia ya marehemu Rukara ilikataa ofa hiyo na …

hali ya vuta nikuvute ikaanza

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, wanaohusika na uuzaji wa nyumba ya marehemu Mohammed Rukara walimweleza mjumbe wa Waziri Mkuu kuwa hiyo ndiyo bei ya mwisho na hivyo hawawezi kushuka chini ya bilioni nne. Waziri Mkuu Gervais Ndirakobuca almaarufu Ndakugarika akaapa kwamba “atawaonyesha kile ambacho ana uwezo wa kukifanya” kulingana na vyanzo vyetu. Moja wapo mwa maamuzi aliyoyafanya siku chache baadaye kwenye makazi ya familia hiyo ni …

… kukatwa kwa miti yote

Kwa zaidi ya wiki moja, Waziri Mkuu ameleka watu waliokua na kazi ya kukata miti yote kwenye makazi ya familia ya marehemu Mohammed Rukara. Hii ni pamoja na miembe, ndimu, miparachichi na michungwa. Kulingana na vyanzo vyetu, Gervais Ndirakobuca alieleza kuwa miti hiyo ilihifadhi mbu ambao waliwauma mapolisi wake.

Hadi Ijumaa hii, shughuli ya ukataji miti hii iliyoanza Alhamisi asubuhi ya wiki iliyopita, ilikuwa bado haijaisha kwa sababu miti hii ilikuwa mingi sana na mikubwa mno kwenye nyumba hiyo ya aliekua Msuluhishi wa kwanza wa taifa la Burundi aliyefariki mwezi Novemba 2019.

Tulimpigia simu Waziri Mkuu wa Burundi Gervais Ndirakobuca mara kadhaa lakini hakupokea simu yake ya mkononi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *